Washiriki wa maonyesho ya kilimo ya mwaka huu mjini Mombasa wamelalamikia utaratibu uliowekwa kuandaa tamasha hilo.
Washiriki hao wamelalamika kuhusu tarehe na wakati ambapo maonyesho ya mwaka huu yaliandaliwa, ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Wakizungumza katika uwanja wa Mkomani siku ya Alhamisi, baadhi ya washiriki hao walisema kwamba kawaida maonyesho hayo huandaliwa wakati wa likizo ambapo shule huwa zimefungwa na wanafunzi huwa wengi katika sherehe hizo.
“Wanafunzi wa shule huwa wanachangia pakubwa sana katika sherehe hizi. Wao ndio huja kwa wingi na hata pia kufanya tamasha hili liwe la kufana, lakini mwaka huu wametuangusha kabisa,” alisema Francis, mmoja wa washiriki hao.
Aidha, walisema kwamba huenda waandalizi wa tamasha hilo wasifikie viwango vya mapato walivyokuwa wametharia kufikisha hapo awali.
Idadi ndogo ya watu ilionekana katika uwanja huo tangu maandalizi yalipoanza, huku baadhi ya viti vikionekana kuwa vitupu wakati wa hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta.
Maonyesho ya kimataifa ya kilimo mjini Mombasa yalikuwa yameratibiwa kuanza tarehe Agosti 24, ambapo shule bado zilikuwa zimefungwa, lakini kamati ya andalizi ikabadilisha tarehe hadi Agosti 31, wakati ambapo wanafunzi walikuwa wakijitayarisha kurudi shuleni.
Washiriki wa mwaka huu ambao wengi wao wameleta bidhaa mbalimbali za kilimo kwa maonyesho hayo, wameitaka kamati andalizi ya maonyesho hayo kujifunza kutokana na hali hiyo ili wasirudie jambo hilo katika miaka inayokuja.
Maonyesho hayo yaliyofunguliwa rasmi siku ya Alhamisi na Rais Uhuru Kenyatta yanatarajiwa kukamilika Jumapili.