Mahakama moja jijini Mombasa imeagiza vijana 17 walionaswa kwa tuhma za uhalifu na wizi katika eneo la Majengo kuzuiliwa kwa siku tano hadi uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni baada ya afisa wa upelelezi, Safari Chea, kuitaka mahakama kumpa muda zaidi wa kukamilisha uchunguzi wake.

Chea aliwasilisha ombi hilo mahakamani siku ya Jumatatu na kusema kuwa anahitaji muda ili kuwapa walalamishi fursa ya kuweza kuwatambua wahalifu hao.

Afisa huyo wa upelelezi aliwataja vijana hao kuwa tishio kwa jamii ya maeneo hayo, ikizingatiwa wanadaiwa kuwahangaisha wananchi.

Wakili wa washukiwa hao Jerad Magolo alipinga ombi la kuzuiliwa kwa vijana hao na kuitaja hatua hiyo kuwa kinyume cha sheria na ukiukaji wa haki za mtuhumiwa.

Hakimu katika mahakama ya Mombasa, Irine Ruguru alikubali ombi la afisa wa upelelezi na kuagiza washukiwa hao kuzuiliwa kwa siku tano katika Kituo cha polisi cha Makupa.

Vijana hao walitiwa mbaroni siku ya Jumapili katika maeneo ya Buxton, Tononoka na Majengo wakiwa na mapanga na visu vinavyoshukiwa kutumika katika kutekeleza uhalifu.