Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Washukiwa waliozuiliwa rumande katika gereza la wanawake la Shimo la Tewa wameitaka idara ya mahakama kuhakikisha kwamba kesi zao zinasikizwa haraka.

Washukiwa hao wamesema kuwa zoezi la kufanya uchunguzi huchukua muda mrefu, jambo linalowafanya kukaa siku nyingi korokoroni.

Wakizungumza na mwandishi huyu alipozuru gereza hilo siku ya Ijumaa, washukiwa hao walisema kwamba ni kinyume cha sheria kukaa korokoroni kwa muda mrefu bila ya kuhukumiwa.

“Baadhi ya washukiwa wamekaa hapa kwa miaka mitatu, na wengine hata miaka minne, na bado kesi zao hazijafikia uamuzi,” alisema Debra Chika, mmoja wa washukiwa hao.

Wakati huo huo, wameitaka idara hiyo kupunguza kiwango cha dhamana kinachotozwa na mahakama, kwa kusema kuwa wengi wao hawana uwezo wa kifedha.

Hilda Mwangome, ni mmoja wa washukiwa hao ambaye alishtakiwa kwa kosa la kushindwa kulipa deni la rafika yake la shilingi elfu 40.

Mwangome alisema kuwa aliamuriwa kulipa dhamana ya shilingi laki moja ambayo hakuweza kulipa kwani familia yake ni maskini.

“Sasa kama nimeshtakiwa na deni la shilingi elfu 40, kisha tena naitishwa laki moja, nitaitoa wapi wakati hata nyumbani sijui wanakula nini?” aliuliza Mwangombe.

Vile vile, washukiwa hao walisema kuwa changamoto nyingine inayowakumba ni mashahidi kukosa kufika mahakamani wakati wa kesi, na hivyo kuwafanya wao kurudishwa korokoroni.

Kwa upande wake, Hakimu katika Mahakama ya Mombasa Douglas Ogot alisema kuwa kuna kesi nyingi ambazo zimesalia katika faili zao, lakini akaahidi kushirikiana na wadau kuzimaliza.

“Tutajaribu tuwezavyo tushirikiane na waendesha mashtaka walete mashahidi ili tumalize kesi hizo kwa muda unaofaa,” alisema Ogot.