Washukiwa wanne wanaohusishwa kuwa wanachama wa kundi la Al-shabab watazidi kusalia korokoroni hadi Aprili 25, 2016 kusubiri kupewa dhamana.
Kassim Ali Ahmed, Mohamed Kassim, Ali Mohamed Bwanad na Mustafa Kheri wanadaiwa kuwa na uhusiano na kundi la Alshabab.
Aidha, wanne hao wanakabiliwa na madai ya kupatikana na bunduki moja na risasi 7 katika eneo la Majengo mnamo Januari mwaka huu.
Haya yanajiri baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa, siku ya Ijumaa, kuiambia mahakama kuwa wanataka kuchanganya kesi hiyo na nyingine sawia na hiyo kabla ya kupewa dhamana washukiwa hao.
Mwendesha mashtaka Erick Masila, aliambia mahakama kuwa wanapinga kuachiliwa kwa dhamana kwa washukiwa hao ikizingatiwa wanakabiliwa na mashtaka mazito.
Kesi hiyo ilikuwa mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Mombasa Susan Shitub.