Washukiwa wanne wa ugaidi watasalia korokoroni kwa siku tatu wakisubiri uchunguzi kukamilika.
Ali Musa Mwadzala, Hamisi Hakim Bwanaidi, Yasin Ahmed Kipsandui na Mwinyi Mwabondo Musa wanadaiwa kuwa wanachama wa kundi la ISIS na al-Shabaab.
Haya yanajiri baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma kuomba muda zaidi wa kukamilisha uchunguzi wa kesi hiyo, kabla ya kuwafungulia mashtaka.
Akiwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Julius Nange’a siku ya Jumanne, mwendesha mashtaka Lydia Kagori alisema uchunguzi huo ni wakina na unahitaji zaidi ya siku 14.
“Uchunguzi wa kesi hii ni wa kina na unahitaji umankinifu kwani itabidi tuchunguze simu za washukiwa hao wanne,” alisema Kagori.
Aidha, ameongeza kuwa itawalazimu maafisa wa uchunguzi kusafiri hadi nchini Somalia kuchunguza uhusiano wa washukiwa hao na mitandao ya ugaidi.
Hatua hiyo ilipingwa na wakili wa washukiwa hao, Chacha Mwita, aliyesema kuwa hiyo itakuwa ukiukaji wa haki za watuhumiwa.
“Hii ni njama ya kukandamiza haki za washukiwa. Kwani nini polisi wasingefanya uchunguzi kabla ya kuwatia mbaroni?” aliiliza Chacha.
Chacha alisema kuwa wateja wake walikamatwa tarehe Oktoba 7, 2016 wakiwa katika jengo la Mahakama ya Mombasa, walipokuwa wamehudhuria kikao cha kesi ya jamaa wao.
“Wateja wangu walitiwa mbaroni juma lilopita wakiwa wamehudhuria kikao cha kesi mahakamani. Je hatua hiyo inamaanisha kwamba familia za washukiwa hawafai kuhudhuria vikao vya mahakama?” aliuliza Chacha.
Aidha, amewalaumu polisi kwa kuwafikisha wateja wake mahakamani baada ya masaa 24.
Hakimu Nange’a ameagiza washukiwa hao kuzuiliwa katika Kituo cha polisi cha Port kwa siku tatu badala ya siku 14.
Kesi hiyo itatajwa siku ya Ijumaa kubaini iwapo uchunguzi umekamilika.