Washukiwa wawili wa mauaji ya watu 12 huko Hindi Kibokoni, wameachiliwa huru baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma kushindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha.
Swaleh Shebe Auni na Joseph Chege wanakabiliwa na kesi ya mauwaji ya watu 12 huko Hindi kaunti ya Lamu mnamo Julai 5, 2014 na Julai 6, 2014.
Akitoa uamuzi huo siku ya Jumanne, Jaji Martin Muya kutoka mahakama ya Mombasa, alisema kutokana na ushahidi wa mashahidi 34 wa serikali ni wazi kuwa wawili hao hawakuhusika katika mauwaji hayo ya Hindi.
Itakumbukwa Swaleh Shebe alitokwa na machozi mbele ya mahakama kuu alipokuwa akielezea mahakama jinsi alivyopigwa sehemu za siri na maafisa wa KDF.
Aliongeza kuwa alipelekwa msituni na maafisa wa KDF na kupigwa sehemu zake za siri, huku akilazimishwa kukubali kuhusika na mauwaji hayo.
Aidha, alisisitiza kuwa wenzake wawili walipigwa risasi hadi kufariki na wanajeshi hao.