Watu 35 walifikishwa katika korti ya munispaa ya Eldoret hapo jana wakiwa wameshtakiwa kwa makosa mbali mbali.
Washukiwa 21 walishtakiwa kwa makosa ya kupiga kelele na kuvuruga amani baada ya kulewa katika mji wa Eldoret.
Wengine 14 walishtakiwa kwa kosa la kutengeneza na kuuza pombe haramu bila leseni katika mitaa ya Langas, Moi’sbridge, Yamumbi, Tegeldich, Merewet na Road block yote ikiwa ni katika Kaunti ya Uasin Gishu. Operesheni ilifanywa na polisi wa utawala siku ya Jumamosi na Jumapili.
Kati yao ni watu wanne ambao walikua wakichuuza jana asubuhi katikati mwa mji wa Eldoret na walitiwa mbaroni na askari wa munispaa.
Aidha washukiwa hao walitozwa faini ya Sh1,300 kwa wale waliokua wakipiga kelele ili kuwa mfano kwa wale wenye tabia kama hizo huku 14 wakitozwa faini ya kati ya Sh12,000 na Sh45,000 mtawalia.
Wachuuzi hao waliopatikana na hatia walihukumiwa kufanya kazi kwa jamii siku kutwa kisha kuachwa huru.
Pombe iliyonaswa ilikua zaidi ya lita 150 na ilikua aina ya kangara, busaa na chang’aa. Hukumu hiyo iliyotolewa mwendo wa saa sita mchana ulitolewa na hakimu makazi wa korti ya munispaa hiyo N.N Moseti.