Vijana wawili wanaoshukiwa kuwa magaidi watasalia rumande kwa muda wa siku 23 wakisubiri uchunguzi kukamilika.
Julius Sifa Yaa na Moses Kosgei walitiwa mbaroni mnamo Disemba 20 na 21 mtawalia katika eneo la Mvita, jijini Mombasa.
Wawili hao walipatikana na kanda zenye mafunzo ya kigaidi ya kundi la al-Shabaab.
Afisi ya mwendesha mashtaka ilitoa ombi kwa mahakama siku ya Ijumaa kuwazuia wawili hao kwa muda wa wiki tatu hadi uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.
Hakimu Francis Kyambia alikubali ombi hilo na kuagiza Yaa kuzuiliwa katika kituo cha Nyali, huku Kosgei akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Bamburi.
Kesi hiyo itasikizwa Januari 13, mwaka ujao.