Washukiwa watatu waliodaiwa kuwa wanachama wa makundi ya kigaidi ya ISIS na al-Shabaab wameachiliwa huru bila masharti.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Washukiwa hao, Ali Musa Mwadzala, Hamisi Hakim Bwanaidi, na Mwinyi Mwabondo Musa, waliokuwa wametiwa mbaroni mnamo Oktoba 7, 2016, waliachiliwa huru siku ya Ijumaa.

Uamuzi huo uliafikiwa na mahakama baada ya kiongozi wa mashtaka, Lydia Kigori, kuthibitisha kutokuwepo kwa ushahidi, kulingana na ripoti aliyoiwasilisha mahakamani kutoka kwa kitengo cha polisi wa kukabiliana na ugaidi ATPU.

Hata hivyo, Bi Kigori amemtaka mshukiwa wa nne, Yasin Ahmed Kipsandui, kuwasili katika Kituo cha polisi cha Ukunda mara moja kwa wiki kwa muda wa mwezi mmoja, kwa ajili ya uchunguzi.

Kigori alisema kuwa bado simu ya Yasin inafanyiwa uchunguzi, na huenda polisi wakapata ushahidi dhidi yake.

Aidha, Bi Kigori alitaka Yasin kuendelea kuzuiliwa uchunguzi unapoendelea, jambo ambalo lilipingwa vikali na wakili wake Bw Chacha Mwita.

Akitoa hukumu yake, Hakimu Julius Nang'ea aliwaachilia huru washukiwa hao, huku akimtaka Yasin kupiga ripoti katika Kituo cha polisi cha Ukunda kwa majuma matatu, mara moja kila wiki.