Polisi mjini Nyamira wameanzisha uchunguzi wa kuwanasa washukiwa wa ujambazi waliowapiga risasi na kuwaua walinda usalama wawili wanaodumisha usalama vijijini almaarufu 'vigilante' katika kijiji cha Kiabore kata ya Bokeira kaunti ya Nyamira usiku wa kuamkia Ijumaa. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akithibitisha kisa hicho, chifu wa kata ya Bokeira Joseph Aima alisema waendazao Paul Nyanumba na Nyangaresi Nyamboga walikumbana na mauti pale walipokuwa wakipiga doria kwenye kijiji hicho cha Kiabore saa sita usiku wa kuamkia ijumaa. 

"Waliouawa walikumbana na maafa yao pale walipokuwa wakifanya opereshini ya usalama kwenye eneo la kiabore walipopigwa risasi na washukiwa wa ujambazi," alisema Aima. 

Aima aidha aliongeza kwa kuwahimiza wakazi wa eneo hilo kushirikiana kikamilifu na maafisa wa polisi kwenye uchunguzi wa kuwanasa wahalifu hao.

"Ningependa kuwahimiza wakazi wa eneo la Bokeira kushirikiana kikamilifu na maafisa wa polisi kwenye uchunguzi ili kuwasaidia maafisa hao kuwakabili kwa urahisi wahalifu hao," aliongezea Aima. 

Tayari miili yao imeondolewa kwenye eneo la tukio na imepelekwa kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi mauti cha hospitali kuu ya Nyamira.