Mahakama ya Mombasa imewaachilia huru bila masharti wasichana watatu, waliokamatwa kwa tuhuma za ugaidi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Nastaheno Ali Thalili, Luul Ali Thahil na Zamzam Abdi Abdallah walitiwa mbaroni Septemba 19 na 20, 2016 kwa madai ya kuwa na ufahamu kuhusu shambulizi la Kituo cha polisi cha Central.

Aidha, inadaiwa kuwa wasichana hao walikuwa marafiki wa washukiwa wa ugaidi waliovamia kituo hicho.

Hakimu Henry Nyakweba alisema kuwa afisi ya mwendesha mashtaka haikuwasilisha sababu mwafaka za kuwazuia washukiwa hao korokoroni kwa muda huo wote.

“Hakuna sababu kubwa ya kuwazuia wasichana hawa kwa muda wa siku saba. Polisi wanafaa kufanya uchunguzi kabla ya kuwatia mbaroni washukiwa wowote,” alisema Nyakweba.

Siku ya Jumatano, Kiongozi wa mashtaka Erick Masila aliambia mahakama kuwa polisi wanahitaji muda wa siku saba kuchunguza simu za washukiwa hao.

“Watatu hawa wanashukiwa kuwa na ufahamu kuhusu uvamizi wa kituo cha polisi cha Central,” alisema Masila.

Wakili wa washtakiwa hao Jerad Magolo alipinga ombi hilo kwa kusema hakuna sababu mwafaka ya kuwazuia wateja wake.

“Hatua hiii inakiuka haki za mshukiwa kulingana na katiba na wanapaswa kuachiliwa huru. Kusoma shule moja ama darasa moja na washukiwa wa ugaidi haimanishi kuwa wateja wangu ni magaidi,” alisema Magolo.