Mshirikishi wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa akiwahutubia wanahabari hapo awali. Amesema kuwa serikali haitalegeza kamba katika vita dhidi ya mihadarati. Picha/buzzkenya.com
Maafisa wa usalama eneo la Pwani wamewatia mbaroni walanguzi watano wa dawa za kulevya.
Maafisa hao pia walifanikiwa kunasa kilo 15 za heroini pamoja na shilingi milioni 18 katika oparesheni hiyo.Akizungumza na wanahabari katika kituo cha polisi cha Bamburi, mshirikishi wa ukanda wa Pwani Nelson Marwa alisema kuwa washukiwa hao walitiwa mbaroni katika maeneo tofauti ya Mombasa na Kilifi.Aidha, ameongeza kuwa polisi wako imara kuangamiza biashara hiyo ya mihadarati.“Tutawanasa walanguzi na kamwe hatutalegeza kamba katika vita hivyi dhidi ya dawa za kulevya,” alisema Marwa.Kufikia sasa, washukiwa 17 wa ulanguzi wa mihadarati wametiwa mbaroni, ikiwemo wana wa marehemu Ibrahim Akasha.Marwa amesema kuwa serikali haiwezi kushindwa kukabiliana na walanguzi hao, huku akiwasihi wananchi kushirikiana na idara za usalama ili kukabiliana na tatizo hilo.“Tunawaomba wananchi kutoa habari kwa polisi ili tuweze kuwatia mbaroni walanguzi zaidi,” alisema Marwa.