Polisi katika Kaunti ya Kiambu wanawazuilia washukiwa wawili wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab.
Washukiwa hao walinaswa katika kituo cha magari cha Banana mjini Kiambu siku ya Alhamisi. Mohamed Abdi Mohamed na Mohamed Aden Nur walinaswa wakiwa na Sh25,000 pesa taslimu, kadi kadhaa za simu na flash disc.
Wawili hao hawakuweza kuzungumza lugha ya Kiswahili wala Kiingereza. Walinaswa wakikagua majumba kadhaa mjini humo kwa nia ambayo haijabainika.
Maafisa wa Polisi kwa sasa wameanza uchunguzi kuhusiana na nia ya washukiwa hao. Kundi haramu la Al-Shabaab limekuwa likihangaisha watu hapa nchini na kuua raia wasio na hatia.
Kundi hilo ni miongoni mwa makundi haramu hatari sana ulimwenguni na linapovamia mahali, huacha hasara kubwa vikiwemo vifo.
Ni hivi maajuzi wanamgambo wa Al-Shabaab walikivamia Chuo Kikuu cha Garissa na kuua watu takriban 148 na kuacha wengine wakiuguza majereha.
Tangu kisa cha Garissa, watu wengine haswa wanafunzi hawajulikani waliko hadi wa leo.