Jengo la Mahakama ya Mombasa. [Picha/ the-star.co.ke]
Mahakama ya Mombasa imewaachilia huru washukiwa wawili wa ugaidi baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha dhidi ya madai yanayowakabili.Ahmed Abdalla Ali na Nassir Abdalla Sikanda wanadaiwa kuhusika katika tukio ambalo kilipuzi kililipuliwa katika eneo la Reef Hotel eneo bunge la Kisauni mnamo Mei 3, mwaka 2014.Aidha, wawili hao wanadaiwa kupatikana na begi moja na fulana mbili ambazo zinadaiwa kutumika katika kubebea kilipuzi hicho.Washukiwa hao wamekaa kizuizini tangu kukamatwa kwao mwaka wa 2014 hadi sasa, huu ukiwa ni mwaka wao wa nne korokoroni.Akitoa uamuzi wake siku ya Jumatano, Hakimu mkuu katika Mahakama ya Mombasa Francis Kyambia alisema kuwa afisi ya mwendesha mashtaka imekosa kuwasilisha ushahidi wa kutosha dhidi ya madai yanayowakabili wawili hao.“Afisi ya mwendesha mashtaka imekosa kuwasilisha ushahidi wa kutosha ambao ungewezesha mahakama kuwafunga jela washukiwa hawa," alisema Kyambia.Hakimu Kyambia aidha aliwalaumu polisi kwa kukosa kufanya uchunguzi wa kina katika kesi za ugaidi ambazo alisema hukamilika bila washukiwa kufungwa jela.