Mahakama ya Mombasa imewapata na kesi ya kujibu washukiwa wawili wanaodaiwa kutoa hifadhi kwa mshukiwa wa mauaji ya watu 15 katika Hoteli ya Kikambala Paradise mwaka wa 2002.
Ibrahim Mahafudh Ashur na Luftiya Abubakar Bashrahil wamepatikana na hatia ya kutoa hifadhi kwa mshukiwa wa ugaidi Harun Fazul, baada ya kutekeleza mauaji hayo.
Hakimu Francis Kyiambia amewapata na kesi ya kujibu wawili hao na kusema kulingana na ushahidi uliotolewa, ni wazi walihusika katika kutoa hifadhi kwa mshukiwa huyo.
“Ni wazi kuwa wawili hawa wana kesi ya kujibu, na wanafaa kujitetea,” alisema Kyiambia.
Kesi hiyo itaendelea Septemba 29, mwaka huu ambapo wawili hao watawasilisha mashahidi wao.
Fazul anakabiliwa na tuhuma za kuhusuki na mauaji ya watu 15 katika hoteli ya Kikambala Paradise mnamo Novemba 28, 2002.