Maafisa wa polisi kutoka kitengo cha flying squad Kaunti ya Mombasa wamewapiga risasi washukiwa wawili wa ujambazi katika maficho yao eneo la KCC Miritini, gatuzi dogo la Jomvu.
Akithibitisha kisa hicho, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed alisema kuwa maafisa wa polisi waliendesha oparesheni hiyo siku ya Jumapili katika maficho ya wahalifu hao na kufanikiwa kuwaua wawili hao waliokuwa wamejihami.
Maalim alisema bunduki aina ya G3 pamoja na vifaa vingine vinavyotumiwa na maafisa wa polisi, vilinaswa katika oparesheni hiyo.
“Maafisa wa flying squad walivamiwa maficho ya wahalifu na kufanikiwa kuwaua wawili na kupata vitu kadhaa ikiwemo pingu, sare tatu za polisi miongoni mwa vifaa vingine,” alisema Maalim.
Maalim alisema kuwa bunduki hiyo ya G3 imekuwa ikitumiwa na wahalifu kutekeleza visa kadhaa vya uhalifu.
Aidha, alidokeza kuwa majambazi hao wamekuwa wakisakwa na polisi kwa takriban mwezi mmoja.