Washukiwa wawili wa ulanguzi wa dawa za kulevya wametiwa mbaroni huko Gongoni, Kaunti ndogo ya Magarini, baada ya kupatikana na misokoto kadhaa ya dawa za kulevya.
Akithibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao, afisa mkuu wa polisi wa utawala anayesimamia kitengo cha kushika doria Kaunti ya Kilifi Inspekta Meshack Mwalo, alisema polisi waliwakamata wawili hao, mwanamume mwenye umri wa miaka 20 na mwanamke wa umri wa miaka 40, baada ya kupokea ripoti kutoka kwa umma.
Mwalo alisema wawili hao wanaozuiliwa katika Kituo cha polisi cha Marereni walikamatwa wakiwa na kilo mbili za bangi pamoja na gramu mbili za dawa nyengine ya kulevya ambayo hakuweza kuthibitisha hadi ifanyiwe uchunguzi.
Kulingana na taarifa kutoka kwa wananchi, wawili hao wamekuwa wakiuza dawa hizo kwa muda mrefu, huku afisa huyo akiwarai wananchi kujitokeza na kupeana habari kuhusu walanguzi wa mihadarati ili waweza kukabiliwa kisheria.