Washukiwa wawili wa mafuta ya transfoma waliepuka kifo mapema Jumanne mjini Kikuyu, baada ya umati uliojawa na hamaki kuwashambulia walipowafumania wakikwea mlingoti wa stima.
Washukiwa hao walivamiwa na umati huo kwa kujifanya wafanyi kazi wa kampuni ya umeme nchini, kwa kukwea mlingoti wa stima.
Wakaazi wa eneo hilo waliwashuku wawili hao, kwa kuwa hawakuwa na gari ya kampuni ya umeme, wala sare, kinyume na walivyozoea kuwaona wafanyi kazi wa kampuni hiyo.
Maafisa waliokuwa wakishika doria katika eneo hilo walifika mahala hapo na kuwanusuru washukiwa hao kutoka kwa umati uliokuwa na hasira.
Akidhibitisha kisa hicho, mkuu wa askari Mutene Maweu alisema kwamba wawili hao wanashukiwa walitaka kuiba mafuta ya transfoma, huku akiongezea kuwa wizi wa aina hiyo umekithiri sana, jambo ambalo linachangia katika kukosekana kwa nguvu za umeme kila wakati.
“Wananchi walishangaa ni kwanini wawili hao hawakuwa na gari la kampuni wala sare za kazi, ndiposa waliwashambuliwa wawili hao,” alisema afisa huyo.
“Maafisa wangu waliwaokoa washukiwa hao pasipo na majeraha makubwa na kuwatia mbaroni,”alieleza zaidi.
Aliongezea kwamba wananchi hao walikuwa na hasira kwa kuwa walikuwa wamekuwa na hitilafu za umeme kwa muda mrefu sasa.
Aliwashauri wananchi kuripoti visa vya aina yoyote vya uhalifu kwa polisi, badala ya kuchukuwa hatua mikononi mwao.
Alimalizia kwa kusema washukiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashataka dhidi yao.