Wanafunzi wa kike kutoka Kaunti ya Nyamira wamepata sababu ya kutabasamu baada ya kundi moja la vijana kuanzisha mradi wakusambaza sodo kwa wasichana wanaotoka katika familia maskini.
Akihutubu wakati wa uzinduzi wa mradi huo kule Borabu siku ya Jumanne, mwenyekiti wa shirika la Pillar Foundation, Peter Magaki alisema kuwa shirika hilo liliamua kuanza kusambaza sodo baada ya kugundua kuwa wasichana wengi wamekuwa wakilazimika kuacha shule kutokana na ukosefu wa sodo wanavyostahili kutumia wakati wanapokuwa na hedhi.
"Ni jambo la aibu kusikia kwamba baadhi ya wasichana hulazimika kuacha shule kutokana na ukosefu wa sodo wakati wa hedhi. Hatuwezi kuruhusu hilo kuendelea na ndio maana sisi kama shirika la vijana tumeanzisha mradi wa kusambaza sodo kwa shule zote za umma kwenye maeneo wadi ishirini ya Nyamira. Tutakuwa tukipeana sodo hizo baada ya kila miezi miwili," alisema Magaki.
Magaki alisema kuwa shirika hilo litatumia makanisa mbalimbali kama vituo vya kusambaza sodo hizo, huku akisihi maafisa wa utawala kusaidia shirika hilo kutambua maeneo yaliyo na mahitaji zaidi.
"Tutakuwa tukitumia makanisa kama maeneo ya usambazaji wa sodo na ili kufanikisha hatua hii, tunasihi machifu na manaibu wao kutusaidia kutambua sehemu zilizo na mahitaji makubwa ya sodo," alisema Magaki.