Wasichana wa umri mdogo katika ukanda wa Pwani wameombwa kuwa waangalifu na watu wanaotangama nao ili kuepukana na wavulana wenye nia mbaya kama kuwabaka na kuwapachika mimba za mapema.
Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake Kaunti ya Mombasa Afia Rama amewataka watoto wa kike kujiepusha na watu kama hao na kuhakikisha kuwa wanatangamana na marafiki wema.
Akiongea na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Rama alisema kuwa mara nyingi wasichana ambao wamepitia changamoto ya kubakwa ama kupachikwa mimba za mapema hujikuta katika hali ngumu ya maisha na kuwataka watoto wa kike kuwa makini.
Wakati huo huo, amewataka wasichana kujiepusha na safari za mara kwa mara zisizokuwa na msingi wowote na kuwashinikiza wazazi kuwalinda watoto wao wa kike huku akiitaka serikali kuingilia kati maswala hayo kuzuia kuchipuka kwa visa kama hivyo.
"Kuna haja aya serikali kuingilia kati swala hili na kuhakikisha kuwa washukiwa wa ubakaji wanakabiliwa na kusitishwa ili kuwasaidia watoto wetu kuishi katika hali nzuri ya maisha,” alisema Afiya.
Kiongozi huo ameahidi kuzuru mashinani na kuwaelimisha wasichana wadogo kuhusu umuhimu wa maisha yao na kujiepusha na kutangamana na wavulana wasiowafahamu vyema.