Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Utafiti uliyofanywa na Shirika la Kijamii la ‘Kenya community support centre’ linaloendeleza harakati zake za kuwanasua vijana ili wasijiunge na makundi ya kigaidi limesema kwamba magaidi wanawalenga wasichana kwa kiasi kikubwa.

Chini ya mradi wao wa 'Kataa Kutumiwa', shirika hilo limefichua kwamba kundi la kigaidi la Alshabab limegundua mbinu mpya ya kuwasajili wanawake na kuwateua kama malkia katika kundi hilo, hali inayowafanya wanawake hao kubadili kabisa fikra zao na kujiunga na kundi hilo.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu katika kongamano la vijana linalolenga kuwahamasisha vijana kuhusu athari za kujiunga na kundi hilo la kigaidi, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Phyllis Muema amesema kwamba hali hiyo ni ya kutatanisha.

Aidha, amesema kwamba ni lazima wazazi wawe macho mno hasa katika eneo zima la pwani, la sivyo vijana wadogo wataangamizwa na kundi hilo la kigaidi.

“Utafiti tuliofanya tumebaini kwamba kundi la Alshabab sasa limebadili mbinu mpya ya kuwasajili wasichana na kuwalaghai kuwa watakuwa malkia watakapojiunga na kundi hilo pamoja na kuwapa pesa nyingi. Hali hiyo imekuwa tishio kubwa kwetu na bila ya vijana hawa wa kike kushauriwa basi taifa letu litatumbukia mahali pabaya zaidi,” alisema Muema.

Aidha, Muema alitaka juhudi zaidi zifanywe na idara ya usalama, mashirika ya kijamii, viongozi wa kidini sambamba na jamii yenyewe eneo la Pwani ili kuwakinga vijana dhidi ya kujiunga na makundi ya kigaidi.

Kauli ya mwanaharakati huyo ilijiri siku chache tu baada ya kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa kufichua kwamba wanamgambo sasa wanawalenga wasomi katika vyuo vikuu ili kujiunga na kundi hilo.