Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mvutano baina ya kampuni ya kutengeneza nguo ya EPZ mjini Mombasa na wafanyikazi wake waliosimamishwa kazi hivi majuzi unaonekana kuibua hisia mseto huku kila upande ukijitetea.

Usimamizi wa kiwanda hicho umetoa sababu mbili kuu zilizofanya wafanyikazi hao kusimamishwa kazi mapema mwaka huu.

Katika kikao na kamati ya leba katika kaunti hiyo siku ya Jumanne, kampuni hiyo ilisema kuwa kandarasi yao ya kufanya kazi ilikuwa imekamilika.

Wakati huo huo, pia afisa anayehusika na maswala ya kifedha katika kiwanda hicho Pankaj Mehta alisema kampuni hiyo ilikosa pesa zaidi za kuwalipa kwani mauzo yalikuwa yamepungua.

Lakini madai hayo yalipingwa vikali na wafanyikazi hao waliowahutubia wanahabari siku ya Alhamisi mjini humo muda mfupi kabla kushiriki maandamano.

Wafanyikazi hao walipinga kauli kwamba mauzo yamepungua katika kiwanda hicho na kudai kuwa nguo zilikuwa zikinunuliwa kila siku ishara kuwa biashara ilikuwa shwari.

Aidha, wafanyikazi hao walidokeza kuwa hatua hiyo iliafikiwa punde baada ya wao kujiunga katika muungano wa kutetea wafanyikazi.

Walidai kwamba usimamizi wa kampuni hiyo uliingia wasiwasi baada ya kugundua kwamba wafanyikazi watakuwa na nguvu ya kutetea haki zao za kikazi pindi watakapoingia katika muungano huo.

Wafanyikazi hao walisema kuwa kati ya mambo yaliyowapelekea kujiunga na muungano huo unaofahamika kama ‘Tailors and Textile Workers Union’ ni kufanyishwa kazi zaidi ya muda wa kawaida bila kupewa pesa za ziada miongoni mwa madai mengine.

“Muungano wa wafanyikazi ni muhimu sana na ulikuwa unatusaidia na hata pia sheria ya Kenya inaruhusu wafanyikazi kujiunga na muungano. Kampuni iligundua kuwa tumefunguka macho ndio maana ikatusimamisha kazi,” alisema mmoja wa wafanyikazi hao.

Wataalamu wa sheria za wafanyikazi wanasema kuwa hatua iliyochukuliwa na kampuni hiyo ni makosa kwani kuna utaratibu unaofuatwa kabla wafanyikazi kusimamishwa kazi.

Wakili Yusuf Abubakar, alisema kuwa kampuni inafaa kumpa mfanyikazi fidia kabla kusitisha kandarasi yake kwa ghafla.

“Tukifuata sheria za leba kuhusu hili swala, inabidi EPZ iwarejeshe kazini wafanyikazi wote, na iwapo hiyo itakuwa ngumu, basi iwape fidia kwa sababu hao ni watu wenye familia zao na hawana njia nyingine ya kujikimu,” alisema wakili huyo.