Naibu kamishna wilayani Manga Douglas Mutai amewaonya watahiniwa wanaoendelea kufanya mtihani mkuu wa kitaifa wa KCSE dhidi ya kununua makaratasi bandia ya mtihani huo.
Bwana Mutai amewahimiza wananchi kuwa waangalifu na kuhakikisha kuwa wanaripoti visa aina hiyo kwa maafisa wa polisi.
Akiongea wakati wa sherehe za siku ya Mashujaa siku ya Jumanne kwenye uga wa Uhuru, Mutai alisema kuwa baadhi ya watu tayari wamewalaghai watahiniwa kwa kuwauzia makaratasi bandia.
“Tayari maafisa wa polisi wamemtia mbaroni mshukiwa mmoja aliyepatikana siku ya Jumatatu akiuza makaratasi bandia ya mtihani huo kwa shilingi Sh5,000. Hii ni baada ya kupata fununu kutoka kwa wananchi,” alisema Mutai.
Aidha, Mutai alisema kuwa mshukiwa huyo amezuiliwa kwenye kituo cha polisi mjini Nyamira akisubiri kufikishwa mahakamani punde tu uchunguzi utakapokamilika.