Idadi ya watalii wanaozuru eneo la Pwani inazidi kuongezeka msimu huu ambapo waumini wa dini ya Kikristo wanapojiandaa kusherehekea siku kuu ya Pasaka.
Katika mohajiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumanne, mwenyekiti wa muungano wa wenye hoteli Mkoani Pwani, Sam Ikwaye, alisema kuwa tayari hoteli nyingi zimesajili wageni kati ya asilimia 70 na 80.
Aidha Ikwaye alisema kuwa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hata zaidi ifikapo siku ya Ijumaa ambapo Wakenya wataungana na mataifa mengine kusherehekea siku kuu ya Pasaka.
"Biashara inazidi kuwa nzuri, tayari kuna baadhi ya hoteli ambazo zimerekodi idadi ya wageni kwa salimia mia 100 huku zingine zikitarajia kufikisha kiwango hicho ifikapo siku ya Ijumaa,’’ alisema Ikwaye.
Hata hivyo, Ikwaye alifichua kuwa asilimia kubwa ya watalii ambao wanazuru Mombasa msimu huu ni Wakenya ikilinganishwa na watalii kutoka mataifa ya kigeni.
"Hadi sasa rekodi zetu zinaonyesha kuwa Wakenya ndiyo wamezuru Pwani kwa wingi kuliko wageni wa ugaibuni, ni hatua nzuri na nina wahimiza wazidi kutalii nchi yao,’’ aliongeza Ikwaye.
Aidha aliongeza kuwa idadi ya wageni msimu huu umeimarika pakubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo baadhi ya mataifa ya Ulaya yaliwawekea wananchi wake vikwazo vya usafiri kuja Kenya kufuatia hofu ya kuzorota kwa usalama.
Siku ya Ijumaa waumini wa dini ya Kikristo kote ulimwenguni wanatarajiwa kusherehekea siku takatifu ya Pasaka.