Jengo la Mahakama ya Mombasa.[Picha/ the-star.co.ke]
Wanaume wawili wenye umri wa makamo pamoja na mwanamke mmoja wamefikishwa katika Mahakama kuu ya Mombasa kujibu shtaka la mauaji.Watatu hao, Abdulkarim Musa, Aden Simba na Julie Mamuye wanadaiwa kuhusika katika mauaji ya Moiz Esmail Esmaiji kati ya Novemba 11, 2017 na Novemba 13, 2017 katika eneo la Bombolulu, eneo bunge la Kisauni.Hata hivyo, watatu hao hawakusomewa mashtaka siku ya Alhamisi, baada ya kubainika kuwa hawajafanyiwa uchunguzi wa akili kwa mujibu wa katiba.Jaji Dora Chepkwonyi aliagiza watatu hao kupelekwa katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani kufanyiwa uchunguzi wa akili kabla ya kusomewa mashtaka hayo.Aden Simba alikuwaanatumikia kifungo cha maisha katika gereza la Malindi kwa shtaka sawia na hilo, kabla ya kupelekwa katika gereza la Shimo la Tewa.Simba anadaiwa kupanga njama ya mauaji ya Esmaiji akiwa gerezani.Pascal Nabwana, ambaye ndiye wakili wa Simba, aliiambia mahakama kuwa mteja wake ananyanyashwa katika gereza la Shimo la Tewa, hali aliyoitaja kama ukiukaji wa haki za Simba.Nabwana ameitaka mahakama kuagiza Simba kurudishwa katika gereza la Malindi ambako alikuwa anazuiliwa hapo awali kabla ya kupelekwa katika gereza la Shima la Tewa.“Ni heri mteja wangu arudishwe Malindi kuliko kubaki akiteseka katika gereza la Shimo la Tewa,” alisema Nabwana.Kesi hiyo itatajwa Desemba 13, 2017.