Serikali kuu imehimzwa kutenga fedha zaidi katika kipindi cha mwaka wa fedha kwenye bajeti ya mwaka wa 2016/17 ili kuwaongeza mishahara walimu na maafisa wa polisi nchini.
Akiongea katika mkutano wa kiusalama eneo la Bombolulu mjini Mombasa siku ya Jumanne, Afisa wa nyanjani wa Shirika la kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’, mwalimu Rama amelitaka bunge la kitaifa kuliangazia swala hilo ili kuwawezesha wanafunzi kufanya vyema katika mitihani yao.
Amesema kuwa iwapo serikali itatenga fedha zaidi za kuwaongezea mishahara walimu basi maswala ya migomo ya walimu mara kwa mara itasitishwa na sekta hiyo kuimarika zaidi.
"Tunaitaka serikali kuhakikisha kuwa inatenga fedha za kutosha kwenye bajeti ya mwaka huu kuhakikisha kuwa inawalipa walimu mishahara yao kikamilifu ili kuzuia migomo ya mara kwa mara na kuinua sekta ya elimu kutozoroteka," alisema Rama.
Akijusia swala la umarishaji wa usalama, Rama amesema kuwa lazima idara ya usalama pia itengewe fedha zaidi hasa kushughulikia misharaha ya maafisa wa polisi na mahitaji yao muhimu ili swala la usamlama nchini kuimarishwa zaidi.