Watoto watatu zaidi wanaoushukiwa kuambukizwa homa ya mafua aina ya A na B wamefariki katika hospitali kuu ya Rift valley.
Mkuu wa afya katika kaunti ya Nakuru Mungai Kabii alisema Ijumaa kuwa wanaifanyia miili hiyo uchunguzi kubaini iwapo homa hiyo ndio chanzo cha kifo.
"Ningependa kudhibitisha kuwa tumewapoteza watoto watatu zaidi lakini hatujadhibitisha kuwa vifo hivi vimetokana na maradhi ya Influenza aina ya A na B japo watoto hao walikuwa miongoni mwa waliotengwa kwa wanaougua ugonjwa wenyewe,"alisema Kabii.
Ugonjwa huo hadi kufikia sasa umewaua watoto 39 wenye umri chini ya miaka mitano katika kaunti ya Nakuru na Baringo huku wengine wakilazwa katika hospitali ya mkoa wakiwa na dalili za ugonjwa huo, na ikidhibitishwa kuwa watoto hao waliaga dunia kutokana na ugonjwa huo, idadi hiyo iataongezeka hadi 42 kwa kipindi cha mwezi moja.
Majuzi serikali kwa ushirikiano na idara ya kushughulikia maradhi yanayokurupuka kutoka marekani CDC, iliwatuma maafisa sita kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na kulipuka kwa ugonjwa huo.