Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kaunti ya Nakuru imesema itawasaidia wanafunzi wasio na uwezo wa kuendeleza masomo yao kutokana na matatizo ya kifedha.

Hakikisho hilo lilitolewa na gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua alipokuwa akizungumza kwenye bustani ya Nyayo mjini Nakuru wakati wa kutoa hundi ya shilingi milioni 25 ya ufadhili wa masomo Jumanne.

Huku akiwa ameandamana na naibu wake Joseph Ruto pamoja na baadhi ya viongozi wa kaunti ya Nakuru, gavana Kinuthia Mbugua aidha amesizitiza kwamba atahakikisha watoto kutoka jamii maskini na zisizoweza kugharamia masomo yao watafaidika na hundi hiyo.

Pamoja na hayo, ameweka bayana kuwa serikali yake itaendeleza mpango wa utoaji wa vyakula shuleni ili kuwawezesha wanafunzi kuendeleza masomo yao bila matatizo yoyote.

Wakati huo huo, naibu gavana wa kaunti ya Nakuru Joseph Ruto amesema kwamba serekali ya kaunti ya Nakuru imeweka mipango ya kuakikisha kuwa wafunzi kutoka jamii zisizojiweza katika kaunti hio watapewa sare za shule hivi karibuni.