Mtoto aliyezaliwa nje au ndani ya ndoa sasa ana uhuru wa kutumia jina la babake mzazi bila kutafuta idhini ya mzazi huyo kama ilivyopendekezwa.
Katika uamuzi wake siku ya Alhamisi, Jaji Mumbi Ngugi, alisema kuwa kila mtoto aliyezaliwa ndani au nje ya ndoa ana haki kikatiba kutumia jina la babake mzazi katika cheti chake cha kuzaliwa.
Uamuzi huo unakinzana na pendekezo la mwanasheria mkuu Githu Muigai, kuwa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa asitumie jina la mzazi huyo bila idhini yake.
Kulingana na Jaji Ngugi, hatua hiyo itawapungizia mzigo wanawake kwani itawalazimu wanaume wenye tabia ya kukwepa majukumu na kutelekeza wanao kuwajibika.
Hapo awali, mwanasheria mkuu Githu Muigai, alipendekeza mtoto kutotumia jina la babake mzazi bila ruhusa, ili kuzuia visa vya wanawake kuwalimbikizia wanaume majukumu na lawama kwa watoto wasio wao.
Kuidhinishwa kwa sheria hiyo kunamaanisha kuwa iwapo mwanamume aliye kwenye ndoa atazaa na mwanamke mwingine nje ya ndoa, mtoto huyo atakuwa na haki ya kutumia jina lake katika vyeti vyake vya taifa.