Idadi ya watoto ambao hawaendi shule inaendelea kuongezeka katika tarafa ya Elburgon.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kufuatia haya, wakaazi wa eneo hilo wakiitaka serikali kuwachukulia hatua za kisheria wazazi ambao watoto wao hawasomi licha ya serikali kuwapa fursa ya kufanya hivyo.

Kulingana na wakaazi wa eneo hilo, baadhi ya watoto hao wameacha shule na kwa sasa wameingia mitaani jambo ambalo linazua wasiwasi kuhusu kizazi cha kesho.

Wenyeji hao wakiongozwa na Bw.John Njoroge wamesema watoto hao ambao wanachuma riziki kwa kubeba mizigo sokoni pamoja na kuchota maji wamekaidi agizo la kurudi shuleni huku baadhi yao wakihama makwao na kuishi kwenye vibanda mjini humo.

Njoroge ameongeza kuwa idadi ya vijana wanaorandaranda ovyo mjini Elburgon imeongozeka akisema wengi wa vijana hao wanajihusisha na uharifu ili kupata pesa za kutimiza mahitaji yao.

Wakaazi hao wameuliza utawala wa mkoa kuhakikisha watoto hao wamerudi shuleni na hatua sambamba kuchukuliwa dhidi ya wazazi wanao kiuka haki za watoto kupata Elimu.

Wamesema baadhi ya wafanyibiashara katika tarafa hiyo wanachangia idadi ya watoto hao kuongezeka mjini humo kwa sababu wao ndio wanawapa kazi dogodogo jambo ambalo linawachochea kuacha shule na kujitoza mitaani.

Aidha imefahamika kwamba vijana hao ambao husimama karibu na maduka ya jumla, hoteli na maeneo mengine ya umma hupora wateja bidhaa huku wengine wakiuliza wapita njia kuwapa pesa.