Viongozi kutoka eneo la Limuru katika kaunti ya Kiambu wamesikitishwa na idadi kubwa ya watoto wanaorandaranda mitaani.
Wakiongea siku ya Ijumaa maafisa wa kilimo walipozuru eneo hilo kwa matayarisho ya siku ya wakulima itakayowaleta wakulima pamoja hapo kesho, viongozi hao walisema kuwa idadi ya watoto hao imeongezeka jambo ambalo linawatia wakaazi hofu.
Walisema kuwa suala hili linafaa kutiliwa maanani kabla halijatibuka donda, kwa vile watoto hao wanakuwa kila uchao na hivi karibuni uenda wakajiunga na genge la magaidi.
Mwakilishi wa wadi la eneo la Limuru ya kati, Njenga Murugami akiongea na wanahabari baada ya mkutano huo, alisema kuwa itakuwa muhimu kwa idara ya maswala ya watoto kushirikiana na polisi wa utawala ili watoto hao waondolewe mitanii na warejeshwe makwao.
Alisema kuwa watoto wasiokuwa na mahala pa kuenda watafutiwe makaazi.
Murugami aliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha sana kuwa watoto hao ambao wengine ni wa umri mdogo hawaendi shule, ilhali serikali imetoa elimu ya bure katika shule za msingi.
Kiongozi huyo alitoa wito kwa waziri wa ugatuzi, Ann Waiguru kurejesha mradi wa kusajili watoto wa mitaani katika idara ya vijana ili wapate kunufaika na miradi inayoendelezwa katika kitengo hicho.
Mwenyekiti wa kitengo cha ‘community policing’ katika eneo hilo, John Maina pia alisema kuwa kuwepo kwa vikundi vya watoto vinavyoendeleza uhalifu kunachangia pakubwa na watoto hao wa mitaani.
Aliomba serikali na wakaazi kushirikiana ili kutoa suluhu na kuwaondoa watoto hao mitaani.