Wazazi wote katika kaunti ya Nyamira ambao wanao walikosa chanjo ya Polio wamehimizwa kuwapeleka watoto hao katika hospitali za kaunti hiyo ili kupata chanjo hiyo.
Wito huo umetolewa ili kila mtoto aliye chini ya miaka mitano kupata chanjo hiyo kama njia moja ya kuzuia kuathirika na ugonjwa huo katika siku zijazo.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Nyamira wakati alikuwa anatoa ripoti kuhusu zoezi hilo ambalo lilikamilika wiki jana, daktari mkuu katika kaunti ya Nyamira Jack Magara aliomba wazizi ambao wanao walikosa chanjo hiyo ya Polio kuwapeleka katika hospitali ili kupata chanjo hiyo.
Wakati huo huo, Magara alipongeza wazazi wa kaunti hiyo kwa kujitolea kwao kuhakikisha watoto wao wamepata chanjo, huku akisema idadi waliolenga ilipita.
“Tulikuwa tunalenga kutoa chanjo kwa watoto 130,000 lakini tuliwachanja watoto 135, 643, idadi iliyopita ile tulilenga, kumanisha wakazi wa kaunti hii wanajua umuhimu wa chanjo ya polio,” alisema Jack Magara.
“Wale ambao watoto wao hawakupata chanjo nawaomba wawalete katika hospitali zetu za kaunti ili kupata chanjo hiyo,” aliongeza Magara.