Wachuuzi wa bidhaa mbalimbali mjini Kisii wamewalaumu baadhi ya watoza ushuru katika mji huo kwa kuwatoza ushuru nyakati za asubuhi na kuwafurusha kutoka mahali wanapofanyia biashara zao nyakati za mchana wakidai kuwa wanasababisha msongamano mkubwa.
Wachuuzi hao walidai kuwa wanafurushwa ata ingawa wametozwa ushuru hivyo basi wanaomba serikali ya kaunti ya Kisii kuwapa usaidizi ili kuwanusuru kutokana na unafiki wa watoza ushuru hao.
Wakizungumza na wanahabari mjini Kisii wachuuzi hao wakiongozwa na Mary Morara waliwalahumu watozaji ushuru hao kwa kuwakandamiza.
“Kila siku asubuhi tunalipishwa ushuru na inapofika mchana tunafurushwa kwa kile kinachosemekana kuwa tumeleta msongamano mjini,” alisema Morara.
"Je wakati wanatuitisha ushuru nyakati za asubuhi hawafikirii msongamano? Hatutakubali na tunaomba serikali ya kaunti kuingilia kati,” aliongeza Morara.
Hezron Mokua mchuuzi mwingine pia aliomba kaunti kuwatengea wachuuzi sehemu yao ikiwa serikali imeona wanaleta msongamano mjini Kisii ili nao kuendelea na biashara zao.