Abiria 15 wamejeruhiwa vibaya na wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya wilaya ya Molo na ile ya Mkoa mjini Nakuru baada ya basi walimokuwa wakisafiria kuhusika kwenye ajali katika eneo la Kibunja kwenye barabara kuu ya Nakuru- Eldoret.

Share news tips with us here at Hivisasa

Basi hilo la kampuni ya RENCOM lilikuwa limebeba abiria 33 kutoka Nairobi kuelekea Busia kabla ya kupoteza mwelekeo na kubingiria mara kadha karibu na kituo cha biashara cha kibunja.

Wananchi pamoja na maafisa wa trafiki kutoka kituo cha polisi cha Molo walisaidiana kuwapeleka hospitalini abiria waliojeruhiwa katika ajali hiyo iliyopelekea msongamano mkubwa wa magari.

Kwa mujibu wa abiria ambao walinusurika bila majeraha, basi hilo lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi na huenda dereva hakuwa na uzoefu wa kuendesha gari kwenye barabara hiyo.

Aidha dereva huyo alipigwa na manusura hao waliomkemea kwa kuendesha basi hilo bila kujali wakisema walianza kulalamikia kutokuwa makini kwa dereva huyo tangu walipoanza safari.

Maafisa wa polisi wanaendelea kumsaka dereva huyo ambaye alitoweka baada ya kujinasua kutoka kwa kichapo alichopatilizwa.

Kamanda wa trafiki wilayani Molo Richard Masinde amewasihi madereva kuwa makini na kuzingatia kanuni za usalama barabara ili kupunguza ongezeko la Ajali.Basi hilo lilikokotwa hadi kwenye kituo cha polisi cha Molo.