Jumla ya watu 23 wanatibiwa katika hospitali ya kaunti ya Nakuru, baada ya kuhusika kwenye ajali Jumatatu.
Ajali ya kwanza ilitokea mwendo wa saa kumi alasiri katika eneo la Soilo kwenye barabara ya Nakuru Eldoret, na kuhusisha basi lililokuwa likitoka Magharibi mwa Kenya kwenda Nairobi.
Watu 18 waliopata majeraha walipelekwa katika hospitali hiyo kuu kupokea matibabu.
Ajali ya pili ilitokea katika eneo la Mukinyai karibu na kituo cha kibiashara cha Salgaa, na kuhusisha basi na watu watano walijeruhiwa kwenye ajali hiyo.
Hayo yanajiri huku maafisa wa trafiki wakifanya msako dhidi ya magari yanayokiuka sheria za barabara kwenye barabara kuu ya Nakuru kwenda Eldoret.
Watu saba waliangamia kwenye barabara hiyo tangu mkesha wa mwaka mpya.