Msako dhidi ya pombe haramu mjini Naivasha haswa lokesheni za Mirera-Karagita na Hells Gate bado unaendelea huku wagema watano wakikamatwa siku ya Jumamosi.
Chifu wa Mirera-Karagita Hassan Nguyo na naibu wake walishirikiana na viongozi wa 'Nyumba Kumi' katika eneo hilo kuongoza oparesheni hiyo. Alisema kuwa wauzaji wa pombe haramu walikuwa wanarejela biashara hiyo kwa kubuni mbinu mpya.
Chifu Hassan amesema zaidi ya lita 30 za chang’aa zilipatikana, pamoja na kiasi kisichojulikana cha busaa.
“Siku hizi wauzaji wamegundua njia mpya za kuficha pombe. Leo tulipata ikiwa imewekwa kwenye karatasi kama zile za kuwekea mgonjwa maji hospitalini, kisha zinatumbukizwa kwenye mtungi na hatimaye mtungi huo unaoshwa kwa sabuni ya omo ama unapuliziwa manukato ili kuficha harufu ya pombe," alisema.
Watano hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Naivasha.
Hata hivyo chifu huyo amepongeza idara ya mahakama, akisema kwa sasa kuna wauzaji watatu ambao walikamatwa wiki jana, ambao bado wako korokoroni.
“Mmoja alipigwa faini ya shilingi elfu 110, akashindwa kutoa na bado yuko ndani. Wa pili alipigwa faini ya shilingi elfu 28, na pia yuko ndani," chifu huyo alieleza.
Kulingana na mwenyekiti wa nyumba kumi eneo hilo Hassan ole Narangai, waliamua kuendeleza oparesheni hiyo kila mara kwa sababu akisema kuwa ni vyema kukabiliana na wauzaji hao wa pombe haramu kikamilifu.
“Ninatoa wito kwa serikali kutafuta njia ambayo watu hawa wanavyoweza kurekebishwa kitabia, ili waache kuona kwamba pombe ina pesa za haraka, ilhali inaua wakenya wenzao. Wengine wao hutoa pombe hii Magharibi mwa Kenya, na kuileta hapa Naivasha,” chifu Hassan alisisitiza.
Hayo yanajiri wakati ambapo mwenyekiti wa bodi ya kukabiliana na dawa za kulevya na pombe nchini Nacada, John Mututho, amesema bodi hiyo inahitaji pesa zaidi za kukabiliana na mihadarati.