Watu saba wamepoteza maisha yao huku watu watano wakipata majeraha mabaya katika ajali ya barabarani eneo la Ngata kwenye barabara kuu ya Nakuru kuelekea Eldoret.
Ajali hiyo ya mwendo wa saa tano asubuhi leo ilihusisha trela lilipoteza mwelekeo na kugonga gari aina ya Nissan shuttle lililokuwa likielekea Eldoret.
Fredrick Cherogony ambaye ni mmoja wa wale waliyoshuhudia ajali hiyo na anayeishi karibu na eneo la tukio anasema kuwa dereva wa trela na dereva wa Nissan ni miongoni mwa waliofariki papo hapo kwenye ajali hiyo.
Miili ya saba hao imepelekwa katika ufuo wa kaunti ya nakuru huku watano hao waliyojeruhiwa wamefikishwa katika hospitali kuu ya mkoa wa bonde la ufa kwa matibabu.
Ajali hiyo imetokea saa kadhaa baada ya watu wengine wawili kufariki kwenye ajali nyingine ya barabarani iliyotokea hapo jana mwendo wa saa tano asubuhi katika eneo la greensted viungani mwa mji wa nakuru kwenye barabara kuu ya nakuru kuelekea nairobi, iliyohusisha gari aina ya mini bus lililokuwa na abiria 34 na gari dogo lililokuwa na watu tano.
Miili hiyo ilipelekwa katika ufuo wa umash funeral home viungani mwa mji wa nakuru, huku manusura wakifikishwa katika hospitali ya misheni ya st marys huko gilgil.