Watu wanne walikamatwa na kushtakiwa Jumatatu katika mahakama ya kaunti ya Nakuru kwa makosa mawili ya kutengeneza maziwa yaliyoganda, pamoja na kuendesha biashara bila kibali kutoka kwa idara ya afya.
Wanne hao Mercy Osoro, John Obongi, Miron Richard na Luke Ochieng walifikishwa mbele ya hakimu mkuu Helen Waakivila na kushtakiwa kwamba mnamo tarehe 12 mwezi huu walipatakina katika kampuni ya Optimum eneo la section 58 wakitengeza Yoghurt kwa maziwa yaliyochanganywa na kemikali mbali mbali ikiwemo Peroksaidi ya Hydrogeni.
Kwa mujibu wa cheti cha mashtaka wanne hao walinaswa na maafisa wa afya ya umma ya kaunti ya Nakuru wakiendeleza biashara hiyo haramu.
Hata hivyo mmiliki wa kampuni hiyo Mercy Osoro aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki sita na mdhamini wa kiasi sawa na hicho au pesa taslimu, shilingi laki mbili.
Washtakiwa wengine waliachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu sita kila mmoja huku kesi hiyo ikitarajiwa kusikizwa mnamo tarehe 27 mwezi huu.