Watu watatu walifariki huku mwingine akiendelea kupokea matibabu katika hospitali ya wilaya Molo, baada ya kuhusika kwenye ajali mbaya ya barabara iliyohusisha pikipiki mbili katika eneo la Kangawa kwenye barabara ya Mau Summit kuelekea Molo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kwa mujibu wa kamanda wa idara ya trafiki wilayani Molo Richard Masinde, waliofariki ni mmoja wa madereva wa pikipiki pamoja na abiria wawili.

Masinde ameeleza kuwa pikipiki hizo ambazo zilikuwa zikiendeshwa kwa mwendo wa kasi, zilikuwa zikielekea eneo la Mauche kutoka Bomet, ambapo waadhiriwa walikuwa wameenda kuhudhiria ibada ya mazishi ya mmoja wa Jamaa zao.

Mkuu huyo wa trafiki amesema baada ya pikipiki hizo kugongana katika mteremko huo hatari zilibingiria mara kadhaa na kupelekea wawili wa waadhiriwa kufariki papo hapo, huku mwingine akipoteza maisha yake alipokuwa akielekezwa hospitalini.

Masinde ambaye amesisitiza umuhimu wa usalama barabarani ameuliza madereva haswa wale wa pikipiki kuwa wangalifu na kuheshimu kanuni za trafiki, ili kupunguza ongezeko la ajali.

Amesema vijana wengi wameingilia kazi ya bodaboda bila kutimiza sheria zote za trafiki, akisema kupuuzwa kwa baadhi ya masharti na wahudumu hao wa pikipiki ndio chanzo cha Ajali.

Miili ya watatu hao imehifadhiwa katika mochari ya hospitali ya wilaya Molo, ikisubiri upasuaji huku pikipiki zilizohusika kwenye ajali hiyo zikizuiliwa katika makao ya trafiki wilayani Molo.