Wakaazi wa kitongoji cha Gathe-ini katika eneo la Kianoe kaunti ndogo ya Subukia wangali wana mshtuko baada ya watu wawili kujitia kitanzi kwa muda wa juma moja.
Kwenye visa viwili tofauti, Agnes Wambui Njoroge aliye na umri wa miaka 42 alipatikana Jumatano iliyopita mwendo wa asubuhi na mama yake ambaye walikuwa wakiishi pamoja.
Mwili wa mama huyo wa watoto wawili ulipatikana ukining’inia kwenye paa la nyumba ukiwa na kamba shingoni.
Katika kisa cha pili, kijana wa umri wa miaka 32 alijitia kitanzi jumapili usiku na mwili wake ukapatikana ukining’inia kwa kamba kwenye tawi la mti upande wa nyuma wa chumba chake.
Kulingana na majirani, mwendazake Julius Macharia Wanjiru hakuonyesha dalili zozote za kujitoa uhai na walimfahamu kama mtu mpole asiye penda ugomvi.
“La kushangaza zaidi ni kuwa marehemu Macharia alikuwa na wenzake katika makazi ya marehemu Wambui ambapo walikuwa wakitayarisha pahali watakapo mzika Wambui,” alisema Hezron Kamau ambaye ni mkaazi wa kitongoji hicho.
Naibu chifu wa eneo hilo Monicah Njoroge amedhibitisha visa hivi na kusema kiini cha cha wawili hao kujitoa uhai bado hakijajulikana.
Miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Nyahururu.
Naibu kamishna ya kaunti ya Subukia Jackson ole Chuta alisema katika siku a hivi majuzi kumekuwa na visa vya watu kujinyonga na hali hii ina tisha.
“Huenda vifo hivyo vinachangiwa na hali ngumu ya maisha au matatizo ya kifamilia. Kifo sio suluhisho ya matatizo unayo pitia. Nahimiza kila mmoja awe akitafuta ushauri ili kuepukana na majanga kama haya,” alisema Ole Chuta.