Kulizuka hali ya wasi wasi katika hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha baada ya ripoti kuenea kwamba kuna wagonjwa wawili wamelazwa kwenye hospitali hiyo wanaoaugua kifua kikuu.
Wawili hao na ambao ni wanaume walilazwa kwenye wadi maalum mnamo Jumatatu baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu ulioonyesha kuwa wanaugua maradhi hayo.
Mmoja wao amekuwa akiugua kwa muda ila alikosa kwenda kutafuta matibabu, hadi wakati alikimbizwa kwenye hospitali hiyo baada ya hali yake kudhoofika.
Mgonjwa wa pili ni mwanafunzi wa chuo kikuu hapa nchini, na alikuwa amefika hospitalini akiwa na maumivu ya kifua wakati aligundulika kuwa na maradhi hayo, ila alikataa kufichua chuo anachosomea.
Afisa mkuu katika hospitali hiyo Joseph Mburu alisema wawili hao wanaendelea kutibiwa, na wameona hali yao imeanza kuimarika.
Mburu aliongeza kuwa wawili hao si wa familia moja, na kuongeza kuwa wameweka mikakati mwafaka ili kuhakikisha kuwa wametibiwa bila ya kuambukiza wengine.