Watu wawili wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya wilaya ya Molo, baada ya kuhusika kwenye ajali katika barabara ya Molo – Mau Summit.
Wawili hao, ambao ni dereva wa gari aina ya probox na abiria wake walinusurika kifo baada ya gari hilo kupoteza mwelekeo na kubingiria mara kadhaa.
Kulingana na wananchi walioshuhudia ajali hiyo, gari hilo lilikuwa ikiendeshwa kwa mwendo wa kasi kabla ya kupoteza mwelekeo na kubingiria.
John Njoroge, ambaye ni mmoja wa madereva anayehudumu katika barabara hiyo amesema barabara ya Molo Mau summit iko katika hali mbaya, jambo ambalo linasababisha ongezeko la ajali.
Jesse Mwangi na Eve Njoki, ambao pia ni wakazi wa eneo hilo wamesema ubovu wa barabara hiyo umepelekea wenye magari pamoja na wahudumu wa pikipiki kushuhudia hasara kubwa, huku magari yakiharibika mara kwa mara.
Wamesema kuharibika kwa barabara hiyo ndicho chanzo cha ajali, wakisema wakazi wamekuwa wakishinikiza serikali kuikarabati barabara hiyo ili punguza maafa, pasipo mafanikio yeyote.