Watu wenye kimo kifupi nchini Kenya wanasema kuwa wamekuwa wakipitia changamoto nyingi katika jamii kutokana na maumbile yao.
Kulingana na wao wanasema kuwa hali hiyo imewafanya kukosa fursa muhimu katika maisha kutokana na dhana kwamba hawawezi kutekeleza majukumu mbalimbali.
Mwaka wa 2013 waliamua kuunda chama chao hapa nchini cha kutetea haki zao pamoja na kuangazia mambo wanayopitia kila siku ambapo kwa sasa wanawakilishwa na rais wao pamoja na viongozi wengine kwenye chama.
Akiongea na mwandishi huyu katika mahojiano ya kipekee mjini Mombasa siku ya Ijumaa, rais wa chama cha kutetea haki za watu wafupi nchini Joackim Mwangi alisema kuwa serikali sasa imeanza kutambua haki zao.
“Watu wakituona wanadhani sisi sio watu wa kawaida lakini tunashukuru jamii imeanza kutuelewa na pia serikali imekuwa ikiunga mkono chama chetu.” Alisema Joackim.
Joackim anasema kuwa mara nyingi watu wafupi hukosa nasafi za kazi licha ya kwamba wengi wao wamehitimu kimasomo.
Naye mshirikishi wa chama hicho ukanda wa pwani Hussein Kenga aliambia Hivisasa kuwa alipitia changamoto nyingi kupata elimu kwani wazazi wake hawakutaka aende shuleni alipokuwa mdogo.
Kenga anasema kuwa jamii ya wamijikenda anayotokea ina dhana kwamba mzazi anapozaa mtu mfupi basi uwa ni laana nkatika familia.
“Mimi nilipelekwa shuleni nikiwa na umri mkubwa kwa sababu wazazi waliniweka nyumbani kwanza huku wenzangu wadogo wakiendelea na masomo.” Alisema Kenga.
Kenga mwenye umri wa miaka 46 ana mke na watoto na baada ya kupitia changamoto katika familia hatimaye alifanikiwa kusoma na sasa anajivunia kufanya kazi katika halmashauri ya bandari mjini Mombasa KPA.
Sasa watu wenye kimo kifupi Kenya wanaitaka serikali kupitia kwa hazina ya kufadhili watu wenye ulemavu kuwatambua na kuwapa ufadhili wa kimasomo pamoja na mahitaji mengine ili wajiendeleze na pia waondoe dhana potovu katika jamii.
Chama cha kutetea haki za watu wafupi hapa Kenya kina zaidi ya washiriki 5,000 kote nchini na siku ya Jumamosi wanatarajiwa kufanya maandamano ya amani mjini Mombasa kabla ya kuandaa hafla kubwa ya kutoa hamasisho katika ukumbi wa Tononoka Hall mjini humo.