Baraza la kitaifa la kudhibiti maambukizi ya virusi vya ukimwi NACC, linasema kuwa watumiaji wa mihadarati wanachangia pwakubwa katika usambazaji wa virusi hivyo.
Nacc inasema kuwa utafiti wao umebaini kwamba tabia ya waathiriwa hao ya kutumia sindano moja kujidunga inasambaza virusi hivyo kwa haraka.
Haya yameibuka wakati wa mkutano uliofanyika katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Alhamisi ulioandaliwa na baraza hilo pamoja na shirika la Haki Africa.
Akiongea na mwandishi wetu, mshirikishi wa Haki Afrika Hussein Khalid ameiomba serikali izidishe juhudi za kukabiliana na tatizo la mihadarati ili kukomesha tabia hiyo.
“Watumiaji wengi wa mihadarati hapa Mombasa ni maskini na hawana uwezo wa kumiliki sindano na hiyo ndio sababu wanatumia sindano moja, tunaomba serikali kukabili wasambazaji wakuu wa mihadarati ambao wanawaharibu vijana wetu hapa pwani,” alisema Hussein.
Aidha mwanaharakati huyo amekashifu hatua ya serikali ya kulipua meli zinazoshukiwa kubeba mihadarati akisema jambo muhimu ni kuwatafuta wauzaji wakuu wanaohusika na biashara hiyo.
Mashirika hayo yanasema utafiti unaonyesha watu 3 huambukizwa virusi vya ukimwi kila siku mjini Mombasa huku 2 wakiaga dunia na hivyo kuomba serikali kusihirikiana na mashirika mbalimbali kukabili janga hilo.