Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika linaloshughulikia waathiriwa wa mihadarati Reach Out Trust Pwani limesaidia zaidi ya watu elfu kumi eneo hilo tangu lilipoanza shughuli zake.

Reach Out Trust ilianza shughuli zake mwaka wa 2003 na imekuwa mstari wa mbele kuwasaidia vijana waliotumbukia katika janga la madawa ya kulevya ikizingatiwa kwamba eneo la pwani limeathirika zaidi.

Akiongea afisini zao Mombasa siku ya Jumatatu, mshirikishi wa shirika hilo mjini humo Taib Basheeib alisema kuwa baadhi ya watu waliowasaidia wamerejela familia zao na kuishi maisha ya kawaida.

“Moja kati ya mafanikio yetu ni kwamba wengi wamerudi katika familia zao na hata wengine wamejiunga katika shirika letu na kufanya kazi ya kujitolea,” alisema Taib.

Aliongeza kuwa jamii imekuwa na dhana potovu kwamba mtu anapoingia katika madawa ya kulevywa hawezi akapona.

Kupitia kwa juhudi za shirika hilo, jamii inasisitizwa kuchukua hatua na kuwaelimisha vijana kuhusu madhara ya mihadarati na pia kujitokeza katika mashirika mbalimbali kutafuta msaada.

“Watu wanaamini kwamba mtu akiwa mhathiriwa ni basi maisha yake yameharibika, lakini tungependa kuondoa hizo fikra miongoni mwa wananchi na kueleza kuwa tuna mifano ya watu waliopona.” Aliongeza Taib.

Watumizi wa mihadarati wako katika hatari ya kupata virusi vya Ukimwi hasa wale wanaotumia sindano kujidunga.

Kulingana na shirika la Reachout, tofauti na virusi pia watumizi hawa wanaweza kupata maradhi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kifua kikuu na maradhi mengine yanayotokana na uchafu wa mazingira.

Utafiti kutoka kwa shirika la kudhibiti mihadarati nchini NACADA ni kwamba eneo la pwani lina zaidi ya watumizi mihadarati elfu 60 na idadi hiyo inaaminika kuongezeka kila wakati.