Katibu wa muungano wa wauguzi tawi la Mombasa Peter Maroko, amesema serikali inapaswa kujilaumu kufuatia masaibu yanayoikumba sekta ya afya.
Alisema kuwa wauguzi waliamua kushiriki mgomo baada ya serikali kupuuzilia mbali matakwa yao.
Maroko alisema kuwa wauguzi wamekuwa wakishinikiza serikali kuzingatia mkataba wa nyongeza ya mishahara tangu mwaka wa 2013, lakini hadi sasa Wizara ya Afya imekuwa ikipuuza shinikizo hizo na kuendelea kuwanyanyasa.
Akizungumza Mjini Mombasa siku ya Jumanne Maroko alisema ni aibu kwa serikali kuipuuza sekta ya afya ambayo ni muhimu mno kwa wananchi, na kisha baadaye kuwalaumu wauguzi kwa madai kuwa wamesusia kazi.
“Mgomo huo ndio umeng’oa nanga sasa na utaendelea hadi pale serikali itakapotekeleza nyongeza ya mishahara kwa kati ya asilimia 25-45 kulingana na mkataba,” alisema Maroko.
Hata hivyo, alikiri kwamba mgomo huo umelamaza shughuli za kimatibabu hasa katika hospitali kuu ya Ukanda wa Pwani, ambapo zaidi ya wagonjwa 600 waliokuwa wamelazwa hopsitalini humo wamesalia bila wahudumu.
Maroko aliwashauri wagonjwa kutafuta matibabu katika hospitali za kibinafsi.