Chama cha wamiliki wa vibanda vya maji mjini Mombasa (Mombasa Water Kioski Operation Association) wamemtaka Gavana wa Mombasa Hassan Joho kurejesha huduma za maji kwa wafanyibiashara hao.
Wakiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, wafanyibiashara hao, wakiongozwa na Akinyi Adhiambo walielezea kugadhabishwa kwao na hatua iliyochukuliwa na gavana huyo kwa kuagiza wakatiwe maji pamoja na kubomolewa kwa vibanda vyao vya biashara bila ya notisi.
Wauzaji hao wa maji waliitaja hatua hiyo ya Gavana Joho kama isiyojali maslahi ya mwananchi wa mashinani, huku wakipinga madai kuwa wamekuwa wakiuza maji hayo kwa bei ya juu,
"Tumeghabishwa sana na hatua ya serikali ya kaunti kutukatia maji na kubomoa vibanda vyetu wakidai kuwa ati tumekuwa tukiuza maji kwa bei ya juu. Huo ni uvumi tu unaoenezwa na baadhi ya watu wasiopenda jinsi tunavyofanya biashara zetu,” alisema Adhiambo.
Wafanyibiashara hao aidha wameiitisha mkutano na Gavana Joho ili kutoa lalama zao kwake.
Waliongeza kuwa iwapo atakaidi ombi lao, basi watatumia fursa yao kama wapiga kura kumng’oa mamlakani pindi uchaguzi mkuu utakapowadia.
Mapema mwezi huu, Gavana Joho aliagiza kufungwa kwa vibanda vyote vya kuuza maji kwa tuhuma kuwa wachuuzi hao wamekuwa wakiwauzia wakaazi maji kwa bei ya juu.