Huku bidhaa muhimu ya maji ikiendelea kukosekana katika baadhi ya mitaa ya Mombasa, wauzaji wa maji katika kaunti hiyo wametetea hatua yao ya kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya juu.
Wauzaji hao walisema kuwa wanatembea mbali kutafuta bidhaa hiyo ambapo sasa wanauza kati ya 90 hadi shilingi 100 kila mtungi wa lita 20.
Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumapili katika mtaa wa Kisauni, wauzaji hao wakiongozwa na Saltan Kioko walisema kuwa wanalazimika kutembea hadi eneo la Shika Adabu, eneo bunge la Likoni kutafuta maji.
“Kosa si letu bali wengi wetu hutembea kwa umbali wa hata kilomita kumi kutafuta maji. Mara nyingine tunalazimika kuvuka feri na kuenda ng’ambo nyingine ili kupata maji hayo. Inabidi tuongeze bei kwa sababu wanaotuuzia maji pia wanapandisha bei hivyo basi inakuwa vigumu kwetu kuuza kwa bei ambayo tumekuwa tukiuza,” alisema Kioko.
Kwa siku saba sasa maji yamekuwa nadra kupatikana kwenye jiji la Mombasa, huku wakaazi wengi wakililaumu shirika la kusambaza maji kwa kukata huduma hizo na kuiomba serikali ya kaunti kuingilia kati na kutatua zogo hilo.