Wauzaji wa vyakula katika mabanda mjini Mombasa wamepinga madai ya idara ya afya katika kaunti ya Mombasa kuwa vyakula vinavyouzwa katika mabanda hayo vinachangia kuenea kwa baadhi ya magonjwa miongoni mwa wakaazi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakizungumza na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Jumanne, wenye mabanda hao walisema kuwa wanazingatia usafi katika eneo lao la biashara na kuwa hawajapokea malalamishi yoyote kutoka kwa wanaokula katika mabanda hayo kuwa wameathirika.

‘’Tumefanya biashara ya mabanda kwa zaidi ya miaka mitano, wanaokula hapa hawajawahi lalamika kuwa wameathirika na ugonjwa wowote kwa hivyo tunashangaa kusikia kuwa serikali ya kaunti inataka kufunga mabanda yetu,’’ alisema mmoja wao.

Kilio cha wenye mabanda hao inajiri siku chache tu baada ya Mkuu wa idrara ya afya kaunti ya Mombasa Mohammed Abdi kusema kuwa serikali kaunti itaanzisha msako na kufunga mabanda yasiyoangazia usafi mjini humo.

Kulingana na afisa huyo, hatua hiyo inachukuliwa ili kuthibiti na kuzuia kuenea kwa magonjwa ya homa ya majano pamoja na kipindupindu ambayo tayari yameripotiwa kuzuka mjini Mombasa.