Wachuuzi wa samaki katika soko la Old Town, Mombasa wanasema kuwa biashara yao inakumbana na changamoto kubwa, kwani mashine ya kuhifadhi samaki waliyowekewa na serikali kuu huharibika mara kwa mara.
Wachuuzi hao wanasema mashine hiyo ambayo kwa sasa imeharibika ni kubwa mno na wameshindwa kuirekebisha kwani inahitaji gharama ambayo wameshindwa kumudu, huku wakipendekeza serikali kuwaletea mashine zingine ndogo.
Akiongea na mwandishi wetu siku ya Jumanne katika soko hilo, Omar Athuman ambaye ni mmoja wa wachuuzi hao alisema kuwa kwa sasa wanalazimika kutumia madonge ya barafu kuhifadhi samaki hao.
“Hii mashine amabayo serikali ilituwekea ni kubwa na inapoharibika hatuwezi kuishughulikia. Inatumia pia umeme kiasi kikubwa, afadhali watuletee mashine ndogo kisha watufunze jinsi ya kuzitumia,” alisema Omar.
Awadh Mohamed, mvuvi na pia mshirikishi katika muungano wa wavuvi maarufu kama Old Town BMU aliongeza kuwa serikali kuu pamoja na ile ya kaunti zimekuwa zipuuza kilio chao licha ya kutoa malalamishi.
“Sisi kama wavuvi tunahitaji vifaa maalum vya uvuvi, lakini tunashangaa wizara ya uvuvi hapa Mombasa inafanya nini ilhali uvuvi wa wenzetu Lamu umeimarika, mbona serikali yetu haitujali?” alisema Awadh.
Soko la Samaki la Old Town ni mojawapo ya soko kubwa Mombasa ambapo watu wengi huenda kununua aina mbalimbali za samaki, na wahudumu wake wanasema kuwa matatizo yao yasipo shughulikiwa uchumi utazorota eneo hilo.